Monday, 13 April 2015

WACHEZAJI YANGA WAPEWA TUZO NA MASHABIKI WA FACEBOOK

WACHEZAJI wa Yanga, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wapewa zawadi za pekee na mashabiki
WACHEZAJI wa Yanga, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wapewa zawadi za pekee kwa kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu msimu uliopita.
Wachezaji hao pamoja na wenzao na benchi la ufundi walikabidhiwa zawadi hizo na mashabiki wa Tawi la Facebook lenye makao yake Buguruni jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni baada ya kumaliza mazoezi ya asubuhi kwenye Uwanja wa Karume,
Mwenyekiti wa Tawi la Facebook, Josephat Sinzobakwila ameiambia Goal kuwa wao kama mashabiki, wanafurahi kuona timu ikishinda, lakini pia wanahuzunika kuona timu ikifungwa hivyo ili kuongeza morali wameamua kutoa zawadi.
“Tunahuzunika kama ninyi mnavyohuzunika mnapofungwa, lakini pia tunafurahi kama ninyi mnaposhinda hivyo tumekuja hapa ili kuongeza morali kwa kuwapa zawadi hizi za saa kwa wachezaji wote na kinyango chenye picha ya mtu kwa wachezaji watatu waliofanya vizuri msimu uliopita”, alisema Sinzobakwila.
Sinzobakwila amesema Ngassa alifunga mabao sita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Niyonzima amekuwa mchezaji wa kigeni aliyedumu Yanga muda mrefu kupita wengine na Dida alidaka mchezo kati yao na Azam FC na kuifunga timu hiyo ambayo baadaye ilitwaa ubingwa kwa msimu wa 2013/14.
Hivyo wameona kutoa zawadi pekee kwa wachezaji hao watatu ambazo ni kinyago chenye picha ya mtu na mabango yenye picha zao wakiwa uwanjani.
Ukiachia zawadi ambazo ni maalumu kwa Ngassa, Niyonzima na Dida, wachezaji wengine wote wa kikosi cha Yanga alipewa zawadi ya saa ya ukutani yenye jina lake huku ndani ikiwa na nembo ya Yanga kama ukumbusho.
Baada ya makabidhiano hayo kiungo wa kimataifa raia wa Rwanda Haruna Niyonzima aliiambia Goal anashukuru kwa mashabiki hao kutambua mchango wake kwenye Klabu ya Yanga na kuwaahidi kuendelea kuwapa raha, lakini aliwataka kufahamu kuna bahati mbaya kwa mchezaji kushindwa kufunga bao hivyo wawe wavumilivu inapotokea hali hiyo.

No comments:

Post a Comment