Monday, 27 April 2015

Match Report: Azam FC 4-0 Stand United, Mabingwa wazidi kuwafukuzia Yanga

Ushindi huo unaifanya Azam kufikisho pointi 45 na na kuendelea kujiwekea uhakika wa kumaliza nafasi ya pili msimu huu ili iweze kushiriki michuano ya kombe la Shirikisho mwakani
MAMBO yameonekana kumwendea sawa kocha wa muda wa Azam FC, Mganda George Nsimbe ‘Best’ baada ya leo kuiongoza timu hiyo kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Stand United kwenye mchezo wa Ligi ya Vodacom iliyofanyika uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Matokeo hayo yamerudisha matumaini ya kocha Nsimbe kuendelea kubaki kwenye timu hiyo msimu ujao kwa kua inahitaji kushinda mchezo ujao ili kujihakikishia nafasi hiyo na kupoteza matumaini ya Simba kushiriki michuano ya kimataifa mwaka 2016.
Ushindi huo unaifanya Azam kufikisho pointi 45 na na kuendelea kujiwekea uhakika wa kumaliza nafasi ya pili msimu huu ili iweze kushiriki michuano ya kombe la Shirikisho mwakani.
Winga machachari raia wa Uganda Brian Majwega, alianza kuifungia Azam bao la kuongoza dakika ya 14 akiunganisha krosi ya Salum Abubakar.
Stand United ambayo Jumanne iliyopita iliitoa jasho Yanga licha ya kufungwa mabao 3-2 leo ilikuwa imepoteza kabisa mwelekeo na kucheza bila mpangilio huku mshambuliaji wake tegemezi raia wa Nigeria Abaslim Chidiabele akishindwa kufurukuta mbele ya Pascal Wawa wa Azam.
Mshambuliaji Gaudence Mwaikimba wa Azam aliifungia timu yake bao la pili dakika ya 37, akitumia vyema pasi ya Salum Abubakari tena na hilo kuwa bao la kwanza kwa Mwaikimba tangu kuanza kwa msimu huu.

Azam ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo mawili lakini kocha Nsimbe na Msaidizi wake Dennis Kitambi, walionekana kutoridhika na idadi hiyo ya mabao na kuwahimiza wachezaji wake kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Stand United.
Jitihada za washambuliaji wa Azam zilizaa matunda dakia ya 62 baada ya Mwaikimba kuifungia Azam bao la tatu na lapili kwakwe kwenye mchezo huo akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Stand John Mwenda.
Chipukizi Farid Malik aliyeingia kipindi cha alifunga bao la nne kwa Azam dakika ya 88 na kuipa timu yake ushindi mnono ambao ni wapili kwa msimu huu baada ya ule wa mabao 5-2 dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika Februari sita.
Ushindi huo wa Azam umeendelea kubakisha tofauti ya pointi nne kati yake na Simba ambazo zinawania nafasi ya pili ili kuwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa mwakani.

No comments:

Post a Comment