Thursday 23 April 2015

Simba washinda kwa kishindo, Okwi akidhihirisha yeye ni tegemeo

Katika mchezo wa leo mshambuliaji wakimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi, alifunga hat-trick ya kwanza tangu arejee kwenye timu hiyo akitokea kwa wapinzani wao Yanga
LICHA ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Mgambo JKT leo kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam lakini kikosi cha Simba kina nafasi ndogo ya kumaliza ligi ya msimu huu nafasi ya pili ili iweze kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho 2015.
Ushindi wa leo unaifanya Simba kufikisha pointi 38 huku ikiendelea kubaki nafasi ya pili huku ikiwa imebakiwa na michezo miwili kabla ya kumaliza msimu huu.
Katika mchezo wa leo mshambuliaji wakimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi, alifunga hat-trick ya kwanza tangu arejee kwenye timu hiyo akitokea kwa wapinzani wao Yanga.
Baada ya kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa mabao 2-0 na Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya Simba iliuanza mchezo wa leo kwa kasi na kuandika bao la kwanza dakika ya nane mfungaji akiwa Emmanuel Okwi aliye unganisha krosi ya winga Ramadhani SIngano.
Okwi aliyeukosa mchezo wa Mbeya City, nyota yake ilingara vilivyo kwenye mchezo wa leo baada ya dakika ya 12 kumtengenezea nafasi nzuri mshambuliaji Ibrahim Ajibu lakini kabla mshambuliaji huyo hajapiga kipa wa Mgambo Godson Mmasa aliuwahi mpira huo na kuudaka.
Simba waliendelea kuutawala mchezo huo na dakika tatu baadaye Ramadhan Singano, aliifungia Simba bao la pili dakika ya 15 baada ya kupiga kona iliyoingia yenyewe wavuni na kuzidi kuwavunja nguvu Mbambo ambao katika mchezo wa awali waliifunga Simba mabao 2-0 kwenye dimba la Mkwakwani Yanga.
Baada ya kufungwa bao hilo vijana wa Mgambo walionekana kutulia na kupanga vyema mashambulizi yao kwenye lango la Simba na mara kadhaa washambuliaji Malimi Busungu na Fully Maganga walipoteza nafasi za wazi walizozipata.
Katika dakika ya 34 beki wa Mgambo JKT Ramadhani Maliwa alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Odongo kwa kumchezea vibaya Okwi na mchezaji huyo kulazimika kutolewa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Okwi alirejea uwanjani na dakika ya 42 akaifungia Simba bao la tatu baada ya kutumia uzembe wa mabeki wa Mgambo Bashiru Chanache aliyekuwa ameingia muda mchache kuchukua nafasi ya Abuu Daud na Novatus Lufunga.
Dakika moja kabla timu hazijakwenda mapumziko mshambuliaji wa Mgambo Fully Maganda alipoteza nafasi ya wazi akiwa amebaki na nyavu za lango la Simba lakini cha kushangaza mpira alioupiga uliokolewa na beki wa Simba Juuko Murshid na kufanya timu hizo kwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Simba walikianza tena kwa kasi na iliwachukua dakika tano kuandika bao la nne likifungwa na Okwi tena baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Ibrahim Ajibu na kumlamba chenga kipa wa Mgambo na kufunga kirahisi.
Kocha Goran Kopunovic wa Simba aliwapumzisha Ibrahim Ajibu na Ramadhani Singano na nafasi zao kuchukuliwa na Issa Abdallah na Simon Sserunkuma wakati Bakari Shime wa Mgambo aliwatoa Abuu Daud, Mohamed Samatta na nafasi zao kuchukuliwa na na Sabri Makame na Ayoub Saleh.

No comments:

Post a Comment