TIMU ya wachezaji wakongwe wa Barcelona imeibuka na ushindi wa
mabao 2-1 dhidi ya wakongwe wa Tanzania ‘Tanzania Stars katika mchezo
wakirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye uwanja wa taifa Dar es
Salaam.
Mshambuliajia Luis Garcia ndiye aliyekuwa wa kwanza kuifungia bao la
kuongoza Barcelona dakika ya tisa baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi
ya Kluivert na kumwacha kipa Peter Manyika akiusindikiza kwa macho
mpira.
Wakongwe wa Tanzania Stars walijitahidi kufanya mashambulizi kwenye
lango la Barcelona na dakika ya 44 Yusufu Macho aliisawazishia timu yake
bao hilo kwa shuti kali baada ya kuunganisha mpira uliokuwa umeokolewa
na mabeki wa Barcelona.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya 1-1 huku wageni Barcelona wakiutawala zaidi mchezo huo kwa kufanya mashambulizi mengi.
Kipindi cha pili Barcelona, walikianza kwa kasi na kufanya
mashambulizi mfululizo kwenye lango la Tanzania Stars na washambuliaji
wake Simao Sambrosa na Luis Garcia wakapoteza nafasi nyingi
walizozipata.
Mchezo huo uliendelea kuwa wa kasi na ushindani mkubwa kwa pande zote
mbili kutafuta bao la ushindi lakini walikuwa ni Barcelona
waliofanikiwa kushinda kombe hilo baada ya Patrick Kluivert kufunga bao
la pili kwa penati dakika ya 86. kufuatia Sambrosa kuangusha kwenye eneo
la hatari na Mustapha Hoza ambaye katika mchezo huo alionyesha kiwango
cha juu.
Wachezaji wa Tanzania Stars kama Mohamed Hussein Madaraka Seleman,
Edibili Lunyamila na Dua Said na Bakari Maliwa walijitahidi kuonyesha
uwezo wao wa kupambana na wenzao wa Barcelona lakini walishindwa
kusawazisha bao hilo.
Hiyo nimara ya pili kwa Tanzania Stars kupoteza mchezo wa kimataifa
wa kirafiki kwani Agosti 28 2014 walicheza na timu ya wakongwe wa Real
Madrid na kufungwa mabao 3-1 kwenye uwanja huo wa taifa Dar es Salaam
Tanzania.
No comments:
Post a Comment