HALI bado ni mbaya kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania bara Azam FC baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare
ya 1-1 na Mtibwa Sugar
HALI bado ni mbaya kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania bara Azam FC baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya 1-1 na
Mtibwa Sugar katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Manungu Turiani
Morogoro.
Matokeo hayo yanaifanya Azam kupoteza kabisa matumaini ya kutetea
ubingwa wake msimu huu kwa kufikisha pointi 38 huku vinara wanaoongoza
ligi hiyo Yanga wakiwa na pointi 43 na kesho wanashuka tena uwanja wa
taifa Dar es Salaam kucheza na Mbeya City.
Katika mchezo wa leo Azam ndio walikuwa wa kwanza kuandika bao dakika
ya 17 kupitia kwa nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, lakini dakika
tatu baadaye Musa Hassan Mgosi aliisawazishia Mtibwa Sugar.
Vijana wa kocha George Nsimbe ‘Best’ walijitahidi kupigana kwa ajili
ya kupata ushindi ili angalau kuikaribia Yanga ambayo kabla ya mchezo
huo ilikuwa mbele kwa mchezo mmoja lakini Mtibwa Sugar walikataa kabisa
kuendeleza rekodi mbaya ya kufungwa na Azam nyumbani.
Mshambuliaji Didier Kavumbagu alipata nafasi nzuri dakika ya 68
lakini aliweza kupiga nje huku Musa Mgosi naye akashindwa kuwa na
maelewana mazuri na mshambuliaji mwenzake Amme Ali na hadi mwisho
matokeo kubaki sare.
Kwa matokeo hayo Mtibwa Sugar waliopo nafasi ya 12 wamefikisha pointi
24 lakini bado wanatakiwa kupambana ili kuepouka kushuka daraja
kutokana na matokeo mabaya wanayoendelea kuyapata na sasa imebakiwa na
michezo mitano kabla ya msimu kumalizika.
Leo kabla ya mchezo huo uongozi wa Mtibwa Sugar ulimrudisha kundini
aliyekuwa kocha wa timu hiyo siku za nyuma Salum Mayanga ambaye kwa sasa
ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa ajili
ya kumsaidia kocha wa sasa Mecky Maxime kumshauri mambo ya kiufundi ili
kuinusuru timu hiyo.
Kutokana na mazingira hayo ilitarajiwa mechi ya leo ingekuwa ni ya
ushindani na yenye kashikashi nyingi, lakini katika dakika zote 90 timu
zilicheza mpira wa kawaida.
Baada ya mechi ya leo, Azam wanakwenda Tanga kucheza mechi ya kiporo
Jumatano ya wiki ijayo wakati Mtibwa Sugar wao wanasafiri kwenda Mbeya
kuwavaa vibonde wa ligi kuu, timu ya Tanzania Prisons Jumapili ya wiki
ijayo.
No comments:
Post a Comment