KAMA Yanga ilikuwa na ndoto ya kupata
saini ya straika namba moja wa Simba, Amissi Tambwe wameumia. Friends of
Simba wamesoma mchezo wakaamua kuingia msituni wenyewe.
Kundi hilo lenye wanachama wenye ushawishi mkubwa
kwenye mambo mbalimbali, wanajua kwamba baadhi ya vigogo wa Yanga
wamewahi kufanya mazungumzo na Tambwe kwa siri kubwa wakimshawishi
asitishe mkataba wake na Simba.
Tambwe alitoa masharti matatu ya kutekelezwa ili
arudi Simba msimu ujao ikiwemo kuongezewa mshahara na kuboreshwa kwa
vipengele vya mkataba wake na kulipwa malimbikizo yake ya usajili.
Akizungumza na Mwanaspoti Evans Aveva mmoja wa
vigogo wa Friends alisema wameshaweka mambo yote ya Tambwe sawa imebaki
utekelezaji tu ambao utafanyika baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa
Simba.
Aveva ambaye anagombea nafasi ya Urais katika
uchaguzi ujao wa Simba ameliambia Mwanaspoti kuwa kila kitu kipo sawa na
tangu alipochukua fomu kugombea amepokea simu nyingi za mashabiki ambao
moja ya kazi waliyomtaka kuifanya ni kuhakikisha Tambwe haendi Yanga.
“Unajua tuna uzoefu mkubwa wa mambo ya usajili
katika klabu hii, katika mwaka wa kwanza ni vigumu kumpa maslahi makubwa
mchezaji ambaye ndiyo kwanza anajiunga na timu lakini anapofanya vizuri
kila kitu kinajulikana kwamba kuna haja ya kuongeza vitu vichache
katika kumpa nguvu,”alisema Aveva.
“Tayari tumeshajadili hilo kwa pamoja kila kitu
kitafanyika kwa umakini, atulie maisha mazuri yanakuja tusubiri uchaguzi
umalizike,”alisisitiza. Friends of Simba wamemsimamisha Aveva kwenye
nafasi ya Urais na wamekuwa wakimpa sapoti kubwa ingawa kwenye nafasi ya
Makamu wa Rais wanaonekana kugawanyika.
SOURCE:Mwanaspoti
SOURCE:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment