Thursday, 19 June 2014

WAMBURA ATUPWA RASMI UCHAGUZI SIMBA

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya Michael Wambura kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
 Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana leo (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
 Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
 Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
 Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata kanuni za uchaguzi kama zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani za mara kwa mara.
Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment