WACHEZAJI 11 waliochezea Yanga msimu uliopita wameondolewa kwenye kikosi cha
timu hiyo siku moja kabla ya ujio wa Mbrazil Marcio Maximo.
Yanga inatarajia kumtangaza rasmi Maximo anayetua nchini leo Jumanne kuwa
Kocha mkuu wa timu hiyo lakini kabla hilo halijafanyika wachezaji hao 11
wametupiwa virago vyao kutokana na kutokidhi matakwa ya mahitaji ya bosi huyo
mpya.
Wachezaji walioachwa ni pamoja na Athumani Iddi ‘Chuji’ na David Luhende
ambao walikuwa na namba kwenye kikosi cha kwanza msimu uliopita. Chuji aliingia
kwenye mgogoro na klabu hiyo mwezi Desemba mwaka jana baada ya kuonyesha utovu
wa nidhamu kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe Yanga ilipochapwa mabao 3-1 na
Simba.
Luhende ameenguliwa kutokana na kugoma kuongeza mkataba mapema mwaka huu
walipopatiwa mikataba ya pamoja na wachezaji wengine wa klabu hiyo kwa madai
kuwa mikataba hiyo haikuambatana na marekebisho ya maslahi yao pamoja na fedha
za usajili.
Wachezaji wengine walioachwa ni Hamis Thabit, Yusuph Abdul, Reliants Lusajo,
Shaban Kondo na Ibrahim Job wakati makinda Bakari Masoud, Rehani Kibingu,
George Banda na Abdallah Mguhi ‘Messi’ waliokuwa kwenye timu ya vijana chini ya
miaka 20 nao wakiachwa.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Yanga jana Jumatatu ilieleza kuwa majina hayo
ni orodha ya awali ya wachezaji watakaoachwa kabla ya kuanza kwa msimu
mpya,viongozi wa usajili tayari wameshaanza kutafuta wachezaji wa kuziba nafasi
hizo. Wachezaji wengine walio kwenye hatihati ya kuachwa ni pamoja na Said
Bahanuzi, Jerry Tegete na kipa Juma Kaseja.
Maximo aliiambia Mwanaspoti nchini Brazil kwamba anatua nchini kuisuka Yanga
imara na akasisitiza anataka iwe mfano Afrika. GAZETI LA MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment