Monday 26 May 2014

CECAFA NILE BASIN CUP: AL-MERREIKH WAZOMEWA KWA KUTOKA SULUHU, POLISI `ZENJI MDOBWEDO`, MBEYA CITY `LAIVU` NA AFC LEOPARD USIKU WA LEO

44593hp2Al-Merreikh walizomewa na mashabiki wao baada ya kutoka suluhu jana
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WENYEJI wa michuano ya CECAFA Nile Basin Cup, Al-Merreikh ya Sudan jana wamelazimisha suluhu pacha ya bila kufungana katika mechi ya kundi A dhidi ya Victoria University kutoka Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa habari wa CECAFA, Rodgers Mulindwa, mashabiki wa Al-Merreikh waliwazomea wachezaji wao baada ya kipyenga cha mwisho kupigwa kuonesha kuwa hawajaridhishwa na suluhu hiyo.
Kocha wa klabu Al-Merreikh, Mjerumani, Martin Otto Pfister alikiri kubanwa zaidi na wapinzani wao na kusema kuwa kwa muda wote wapinzani wao waliharibu mipango yao.
“Kiufundi wako vizuri sana (Victoria University). Walicheza kwa jitihada kutunyima nafasi za kushinda. Waliharibu mipango yetu na kutupa nafasi kidogo ya kucheza mpira”. Alisema kocha huyo Mjerumani aliyefanya kazi Afrika tangu miaka ya 90.
Suluhu ya jana imeifanya Victoria University kuwa mshindani wa kombe kwasababu timu zote zimefuzu hatua ya mtoano, huku zote zikiwa na mechi moja mkononi.
Mechi nyingine ilizikutanisha timu za Malakia FC kutoka Sudan kusini dhidi ya Polisi ya Zanzibar.
Kwa mara nyingine tena Maafande hao wa Polisi kutoka kwa ndugu zetu Wazanzibar waliangukia pua baada ya kuburuzwa mabao 3-0.
Mabao ya Makakia FC yalitiwa kambani na Thomas Jacob katika dakika ya 68’, 88’ na la tatu lilifungwa na Richard Justin katika dakika ya 74’.
Kwa matokeo hayo, Malakia wameonesha kuwa bado watakuwepo hatua ya robo fainali, lakini Polisi hawana jinsi zaidi ya kurejea nyumbani baada ya kumaliza mechi yao ya mwisho kesho jumanne.
Mechi nyingine ilipigwa mjini Shandi ambapo Dkhill ya Djibouti ilipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Defence ya Ethiopia.
Matokeo hayo yanawaondoa Dkhill mashindanoni kwasababu kundi moja linatakiwa kutoa timu mbili za kwanza kuelekea katika hatua ya mtoano.
Leo jumatatu na kesho jumanne ni mapumziko mjini Shandi kabla ya wenyeji Al-Shandi kuvaana na Defence siku ya jumatano.
Michuano hiyo itaendelea leo mjini Khartoum ambapo wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo, Mbeya City fc watakabiliana na AFC Leopard kutoka nchini Kenya majira ya saa 2:00 usiku.
Hii itakuwa mechi nyingine ngumu kwa kocha Juma Mwambusi kwasababu Leopard ni timu kubwa na yenye uzoefu wa kutosha katika mashindano makubwa ukanda wa Afrika mashariki na kati.
IMG_8061 (1)Pia hata kihistoria , klabu hii ya Kenya ina muda mrefu zaidi kuliko timu hii changa ya Tanzania.
Hata hivyo, kocha Juma Mwambusi wa Mbeya City fc amesema hakuna haja ya kuwaogopa Leopard kwasababu wao wamejiandaa kupambana kwa mechi zote.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa siku ya jumamosi, Mbeya City fc walishinda mabao 3-2 dhidi ya Academie Tchite ya Burundi.
Mbali na Mechi hiyo ya usiku, mapema saa 11:30 kwa saa za Sudan, Academie watakuwa uwanjani kuoneshana kazi na Etincelles.

No comments:

Post a Comment