Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi tatu mfululizo
KIKOSI cha wekundu wa msimbazi Simba kesho kinatarajia kushuka kwenye
uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga kupambana na wenyeji Mgambo JKT ukiwa
ni mwendelezo wa mechi za ligi ya Vodacom Tanzania bara.
Simba inayonolewa na kocha Mserbia Goran Kopunovic, inaingia kwenye
mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi tatu mfululizo
kwa kuzifunga Tanzania Prisons,Yanga na Mtibwa Sugar.
Mbali ya Simba kuingia kwenye mchezo huo na rekodi nzuri lakini pia
inajivunia kiwango bora na mabao ya kuvutia kutoka kwa mshambuliaji wao
wa kimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi.
Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ya Vodacom ikiwa
na pointi 29 na michezo 18 siku za karibuni imeonyesha kiwango cha
kuvutia na kufufa matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo kwamba huenda
wakatwaa ubingwa au kumaliza nafasi ya pili msimu huu.
Lakini pamoja na kiwango bora walichokuwa nacho Simba kwa sasa
wanapaswa kucheza kwa tahadhari katika mchezo wa leo kwani Mgambo JKT
siyo timu ya kubeza hasa inapokuwa nyumbani na Simba haijawahi kupata
ushindi kwenye uwanja wa Mkwakwani katika misimu mitatu iliyopita.
Mgambo inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi
21 na katika mechi iliyopita iliweza kuifunga Ndanda FC mabao 3-1 kwenye
uwanja huo hivyo Simba isitarajie kupata mteremko.
Kocha Bakari Shime, wa Mgambo JKT, amesema amekiandaa kikosi chake
kwa ajili ya kuikabili Simba na anauhakika wataendeleza wimbi la ushindi
kama walivyofanya kwa Ndanda FC Machi 8.
“Najua Simba ni timu nzuri na kwa sasa wapo kwenye kiwango bora
lakini hatuwezi kukubali kufungwa nyumbani ligi inakwenda mwishoni na
sisi tupo kwenye nafasi mbaya tunalazimika kushinda ili kujiepusha na
janga la kushuka daraja,”amesema Shime.
Kocha Shime ameiambia Goal ataendelea kukitumia kikosi chake kile
kilichoanza kwenye mchezo uliopita akiamini kuwa anaweza kupata matokeo
dhidi ya Simba ambayo kwa sasa inaonekana kuimarika zaidi baada ya
kushinda mechi zake tatu zilizo pita.
Kwaupande wake kocha Goran Kopunovic wa Simba ameonyesha wasiwasi
wake na hali mbaya ya uwanja wa Mkwakwani lakini akaahidi kuzungumza na
wachezaji wake ili waweze kupambana na kupata pointi tatu ili kuendelea
kuzifukuzia timu za Azam na Yanga zilizopo kileleni.
“Uwanja huu ni mbovu mara ya mwisho tulicheza na Coastal Union na
mambo hayakwenda vizuri lakini hatuna namna lazima tucheze nimezungumza
na wachezaji wangu wote kuhakikisha tunapambana kwa dakika zote 90 ili
kupata ushindi,”amesema Kopunovic.
Mgambo JKT huwa na utaratibu wa kukaza kwa kuhakikisha haipotezi
mechi za mzunguko wa pili, hasa zinazochezwa Uwanja wa nyumbani,
Mkwakwani.
Haijawahi kufungwa na Yanga wala Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani
tangu ipande ligi kuu msimu miwili iliyopita na msimu uliopita
ilizifunga timu zote mbili kubwa za Simba na Yanga ilianza na Simba
ikashinda 1-0 na baada ya hapo ikaifunga Yanga 2-1 kwenye uwanja huo.
No comments:
Post a Comment