Thursday 19 February 2015

DANIEL NA REKODI ZAKE LIVERPOOL

hi-res-451546477-daniel-sturridge-of-liverpool-celebrates-scoring-his_crop_exact
Na Augostino Mabalwe kwa msaada wa Mtandao
BAADA ya mkataba wake mwaka 2009 kumalizika katika klabu ya Manchester City,  Daniel Sturridge alitua katika klabu ya Chelsea na kusaini mkataba  wa miaka minne katika timu hiyo iliyokuwa chini ya kocha Carlo Ancelotti.
Sturridge alifunga goli lake la kwanza katika klabu ya Chelsea katika mechi yake ya kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Seattle Sounders ikiwa ni mechi ya kirafiki iliyopigwa tarehe 18 Julai 2009.
15 Septemba 2010 Daniel Sturridge alifunga goli lake la kwanza katika michuano ya klabu bingwa barani ulaya katika mchezo ambao Chelsea walicheza dhidi ya MSK Zullin ikiwa ni mechi yake ya kwanza katika michuano hiyo.
Baada ya kucheza kwa takribani misimu mitatu katika klabu ya Chelsea,Januari 2, 2013 Daniel Sturridge alisajiliwa na klabu ya Liverpool kwa ada ya paundi milion 12.
Daniel Sturridge aliendeleza rekodi yake ya kufunga katika mechi zake za kwanza katika timu na michuano mbalimbali baada ya kufunga dakika ya 7 ya mchezo katika mechi yake ya kwanza katika ushindi wa Liverpool wa 2-1 dhidi Mansfield Town ukiwa ni mchezo wa kombe la FA mzunguko wa tatu uliopigwa Jan 6, 2013.
Mechi yake ya kwanza ya ligi katika klabu hiyo ilikuwa ni dhidi ya Manchester United ambapo aliingia kutokea benchi na kufunga goli lake la kwanza la ligi klabuni hapo licha ya timu hiyo kufungwa 2-1 na mashetani wekundu katika mchezo huo uliochezwa Jan 13 2013.
Sturridge alifunga goli lake la pili la ligi katika mechi yake ya kwanza kuanza katika kikosi cha kwanza cha Liverpool katika ushindi wa 5-0  dhidi ya Norwich Jan 19, 2013 mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Anfield na  kufanya mchezaji huyo kufunga magoli matatu katika mechi zake tatu za mwanzo hivyo kuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kufanya hivyo tangu Ray Kennedy alipoweka rekodi hiyo mwaka 1974.
Msimu wa 2013/2014 aliweka rekodi katika ligi kuu nchini uingereza ya kuwa mchezaji aliyefunga goli la haraka zaidi katika mechi ya ufunguzi ya ligi katika msimu huo,Sturridge aliweka rekodi hiyo baada kufunga goli katika mechi ya ufunguzi ambayo Liverpool waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Stoke City.
Pia katika msimu huu Daniel Srurridge ameendeleza moto wake katika ligi  baada ya kufunga katika mechi ya ufunguzi  ambayo majogoo hao waliibuka na ushindi 2-1 dhidi ya Southampton mchezo uliopigwa katika uwanja wa Anfield na siku chache baadaye mchezaji huyo aliumia wakati akiitumikia timu ya taifa ya England.
Alirejea uwanjani katika mechi dhidi Westham United 31, Jan 2015 na kufunga goli katika mechi hiyo ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu atoke majeruhi.
Leo liverpool itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Anfield kuikaribisha Besiktas ya nchini uturuki katika mchezo wa michuano ya europa na hii itakuwa mechi ya kwanza ya Daniel Sturridge ya michuano ya ulaya katika klabu hiyo baada ya hapo awali kukosa mechi za ligi ya mabingwa barani ulaya kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mguu.
Macho yote ya mashabiki wa Liverpool yataelekezwa kwa Daniel Sturridge kutokana na rekodi zake za kufunga katika mechi zake za kwanza katika michuano mbalimbali

No comments:

Post a Comment