Wednesday 18 February 2015

Southampton yasajili mchezaji wa pili Afrika Mashariki

Mganda aliyesaini SOT
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Baada ya kumsajili Mkenya Victor Wanyama, Southampton FC ya Ligi Kuu ya England (EPL), imesajili mchezaji wa pili kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kumpa mkataba wa miaka miwili na nusu Mganda Bevis Kristofer Kizito Mugabi.
Hata hivyo, beki huyo ambaye wazazi wake wote wawili ni Uganda, ana uraia wa nchi mbili unaomruhusu kuichezea timu ya taifa ya Uganda (Cranes) kwakuwa bado hajacheza katika kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya England.
Mchezaji huyo amekaririwa katika mtandao rasmi wa klabu Southampton FC akisema amefurahi kupewa nafasi ya kukipiga katika klabu hiyo baada ya kuachwa huru na Fulham U18 Julai 2011. Amesema ana matumaini ya kufanya vizuri kwa kujituma kazini.
“Nimefurahi kupata nafasi hii, nimesaini na kila kitu kimekamilika. Lengo langu ni kucheza katika kikosi cha kwanza. Nitafanya kazi kwa bidii mazoezini na wakati wa mechi,” amesema beki huyo mwenye umri wa miaka 19.
“Klabu imenipa nafasi baada ya Fulham kuniacha niende zangu. Hii ni sehemu nzuri kwa mchezaji mchanga. Southampton imetoa wachezaji wakubwa na ninaamini nitakuwa mmoja wao,” amesema zaidi.
England U17
Beki huyo wa kati aliitwa kwa mara ya kwanza katika vikosi viwili vya England U17 lakini hakufanya vyema kutokana na majerha ya goti, amekichezea kikosi cha Fulham mechi nane akifunga mabao matatu yakiwamo mawili katika mechi mbili dhidi ya two Chelsea na Everton.
Anaungana na Jordan Turnbull na Jason McCarthy ambao wote wiki hii wametia saini ya kukipiga katika kikosi cha Martin Hunter cha U21 kabla ya kupelekwa Kikosi A cha Ronald Koeman.

No comments:

Post a Comment