Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Magoli mawili ya mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu na moja la
Muivoru Coast Kipre Tchetche yameirejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Azam FC baada ya kuichapa Kagera
Sugar FC magoli 3-1 katika mechi pekee ya ligi hiyo iliyochezwa leo
Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Matokeo hayo yameifanya Azam FC, iliyopoteza mechi mbili
msimu huu dhidi ya JKT Ruvu Stars na Ndanda FC, ifikishe pointi 20 na
kurejea kileleni mwa msimamo ikifuatwa na wababe Mtibwa Sugar FC wenye
pointi 17 wakiwa ni timu pekee ambayo haijapoteza mechi hata moja msimu
huu.
Nafasi ya tatu inakaliwa na JKT Ruvu Stars yenye pointi 17
pia, mbili mbele ya Yanga SC na Polisi Moro FC waliopo nafasi za nne na
tano. Kagera Sugar FC imeendelea kubaki nafasi ya sita ikiwa na pointi
14. JKT Ruvu Stars, Kagera Sugar FC na Polisi Moro FC wamecheza mechi 11
wakati Mtibwa Sugar FC na Yanga FC wamecheza mechi tisa huku vinara
Azam FC wakiwa wamecheza mechi 10.
Azam, watakaovaana na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Jumamosi, wamekwenda mapumzikoni wakiwa mbele kwa mabao 2-0
yaliyofungwa na Tchetche na Kavumbagu dakika za 3 na 49. Mchezaji Bora
wa Novemba, Rashid Mandawa ameifungia bao la kufutia machozi Kagera
Sugar FC kabla ya Kavumbagu kuongeza la tatu na kuifanya timu hiyo ya
Kagera ipoteze mechi ya pili mfululizo kwenye Uwanja mpya wa CCM
Kirumba.
Kagera Sugar FC inayonolewa na Mganda Jackson Mayanja,
ilipoteza 1-0 dhidi ya Mbeya City FC katika mechi iliyopita kwenye
uwanja huo Jumamosi.
Kavumbagu amefikisha mabao 7 msimu huu akimkimbia Ame Ally
Amour wa Mtibwa Sugar FC kileleni mwa wafumania nyavu hatari msimu huu.
Mandawa naye amefikisha mabao matano sawa na Amour, bao moja mbele ya
Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu Stars, Rama Salim wa Coastal Union FC, Simon
Msuva wa Yanga SC na Danny Mrwanda wa Yanga SC, ambaye hata hivyo mabao
yote manne aliyafunga akiwa na kikosi cha Adolf Richard cha Polisi Moro
FC.
Baada ya mechi dhidi ya Simba SC, Azam FC itakwea pipa kwenda
DRC kushiriki mashindano maalum ya kimataifa nchini humo kabla ya
kuivaa El Merriekh FC katika hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa
Afrika katikati ya mwezi ujao.
Usiku huu El Merreikh iliyotwaa taji la Ligi Kuu ya Sudan
mara 19, inamenyana na timu isiyokuwa na kocha mkuu, KCCA ya Uganda
katika mechi ya kimataifa ya kirafiki inayochezwa mjini Khartoum, Sudan.
Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Uganda KCCA,
Abdallah Mubiru hakusafiri na timu yake hiyo kwenda Sudan kutokana na
kuhudhuria mafunzo ya kozi ya CAF ya ukocha inayoendelea mjini Njeru,
Uganda.
Msaidizi wake John Luyinda ndiye anayekiongoza kikosi hicho
kilichovuliwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kutolewa kwa
penalti robo-fainali na Polisi Zanzibar.
Baada ya mechi ya leo, Meneja wa Azam FC, Jemedari Said
amesema: “Kabla ya hatujaja Kanda ya Ziwa, nilisema tuna malengo ya
kukusanya pointi 9 dhidi ya Stand United FC, Kagera Sugar FC na Simba SC
kabla ya kwenda DRC.”
“Tumemaliza kazi Kanda ya Ziwa, kilichobaki ni kuchukua
pointi kwa Simba SC kabla ya kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa
DRC kujiandaa vyema kwa ajili ya mechi zetu za Klabu Bingwa Afrika mwezi
ujao,” amesema zaidi Jemedari.
Kikosi cha Azam FC leo kimeanza na Aishi Manula, Shomari
Kapombe, Erasto Nyoni, Said Morad, Serge Wawa, Michael Bolou, Mudathir
Yahya/ Amri Kiemba, Frank Domayo/ Gaudence Mwakimba, Didier Kavumbagu,
Kipre Tchetche na Brian Majwega